04.07.03 - ICTR/MILITARY - JAJI WILLIAMS AJIUZULU KUSIKILIZA KESI YA WANAJESHI

Arusha, Mei 23, 2003(FH) Jaji Kiongozi wa Mahakama namba III, katika Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR) amejiondoa katika kusikiliza kesi ya mauaji ya halaiki dhidi ya kundi la kwanza la maafisa wanne waandamizi wa jeshi la Rwanda (FAR) kutokaa na sababu binafsi.

Jaji huyo, George L1oyd Williams kutoka visiwa vya St.

Kitts na Nevis alipoulizwa na shirika la habari la Hirondelle juu ya huo uamuzi wake alisema " siwezi kujadiliana nanyi lolote lile juu ya uamuzi huu. Jaji anaweza kujitoa katika kesi iwapo anataka kufanya hivyo. Ni kutokana na sababu binafsi."

Katikati ya Marchi , mwaka jana, Jaji Yakov Ostrovsky kutoka Russia pia wa mahakama hiyo alijitoa kusikiliza kesi hiyo kwa kile alichoeleza kuwa sababu binafsi.

Hata hivyo Jaji Williams ataendelea kuwa Jaji Kiongozi katika Mahakama hiyo katika kesi ya mauaji ya halaiki dhidi ya maafisa watatu waandamizi wa serikali katika mkoa wa Cyangugu.

Kwa mujibu wa Kofi Afande, Mkuu wa Kitengo Mashtaka na Mratibu wa Mahakama namba III, majopo ya majaji katika mahakama zote tatu yatapangwa upya katika kikao cha pamoja cha Majaji kinachoanza Jumatatu ijayo.

Maafisa wa jeshi waliomo katika kesi hiyo ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Ulinzi, Kanali Theoneste Bagosora, Luteni Kanali Anatole Nsengiyumva, Meja Aloys Ntabakuze na Jenerali Gratien Kabiligi.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Aprili 2, mwaka 2002 na kuahirishwa siku iliyofuata na ikaanza tena kusikilizwa, Septemba 2, 2002 na hatimaye kuahirishwa. Mpaka sasa ni mashahidi wawili tu wa upande wa mwendesha mashtaka kati 250 anaokusudia kuwaleta,  ndiyo waliokwisha kutoa ushahidi wao mahakama akiwemo mpigania haki za binadamu kutoka Marekani, Alison  Des Forges.

Kesi hiyo ambayo inasadikiwa kuwa ni moja kati ya kesi nyeti na muhimu za mauaji ya halaiki inatarajiwa kuendelea kusikilizwa Juni 9 hadi Julai, 18, 2003.

NI/SV/CE/FH (ML'0523t)