Justice Info

TAARIFA ZA HIVI KARIBUNI

07.12.12 - MAJUMUISHO YA WIKI - ANNAN AONYA WAKENYA KUTOWAPA KURA WATUHUMIWA,MSAKO WA VIGOGO WA MAUAJI YA KIMBARI HAUNA MWISHO

Arusha, Desemba 07,2012 (FH) – Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan wiki hii amewataka Wakenya kutowapigia kura wanasiasa wanaokabiliwa na kesi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), huku maafisa waandamizi wa Taasisi Inayorithi Kazi za Mahakama za Kimataifa (MICT) wamesema juhudi za kuwasaka watuhumiwa vigogo watatu wa mauaji ya kimbari zinabakia kuwa kipaumbele cha taaisis hiyo.

ICC

Annan awaonya Wakenya: Jumanne wiki hii, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan aliwataka Wakenya kutowapigia kura wanasiasa wanaokabiliwa na kesi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).Kenya inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu Machi, mwakani.Annan ambaye hivi sasa ni mwangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika (AU) katika uchaguzi huo,alitoa onyo hilo katika ziara yake ya siku mbili nchini humo. Alisema hadhi ya Kenya inaweza kuharibiwa iwapo watuhumiwa wa ICC watapigiwa kura. Watuhumiwa hao ni pamoja na Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta, anayewania urais na Mbunge, William Ruto anayepania umakamu wa rais.

ICTR

Mahakama ya Rufaa kuamua kesi ya mwisho kupelekwa Rwanda mwakani: Jumatano wiki hii, Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Jaji Vagn Joensen alitangaza kwamba Mahakama ya Rufaa itatoa uamuzi hapo mwakani juu ya rufaa ya kupingwa kwa kesi ya mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari,Bernard Munyagishari kwenda kusikilizwa nchini Rwanda. Akiwasilisha taarifa ya ICTR ya kila miezi sita mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jaji Joensen alisema labda kama umuazi juu ya Munyagishari ukiwa ni kinyume chake, Mahakama ya Rufaa itakuwa na jukumu la kushughulikia kesi saba zilizobakia mbele yake ambazo zinatarajiwa kuhitimishwa ifikapo mwishoni mwa 2014.

Vigogo wa mauaji ya kimbari kuendelea kusakwa: Maafisa waandamizi wa Taaisi Inayorithi Kazi za Mahakama za Kimataifa (MICT) Jumatano walisema juhudi za kuwasaka watuhumiwa vigogo watatu wa mauaji ya kimbari zinabakia kuwa kipaumbele cha taaisis hiyo.Rais wa taasisi hiyo, Theodor Meron alikuwa anahutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, ambako alitoa wito kwa wanachama wa Umoja huo kusaidia katika juhudi hizo. Naye Mwendesha Mashitaka wa taasisi hiyo, Hassan Bubacar Jallow alisema harakati za kuwasaka watuhumiwa vigogo wa mauaji ya kimbari akiwemo, Felicien Kabuga anayedaiwa kuwa mfadhili wa mauaji hayo, Waziri wa zamani wa Ulinzi, Augustin Bizimana na Mkuu wa zamani wa Kikosi cha Walinzi wa Rais, Meja Protais Mpiranya,zimeimarishwa. Alisema juhudi hizo hazitakoma hadi hapo watuhumiwa hao watakapotiwa mbaroni na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

WIKI IJAYO    

Kesi ya Bemba kuendelea kuunguruma wiki ijayo: Kesi ya utetezi inayomkabili kiongozi wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Jean Pierre Bemba anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita itaendelea kusikilizwa Jumatatu ijayo, Desemba 10. Uhalifu huo unadaiwa kufanywa kati ya mwaka 2002 na 2003 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mahakama ya Rufaa ICC kuamua juu ya kusikilizwa kwa kesi ya Gbagbo: Jumatano ijayo, Desemba 12, majaji wa Mahakama ya Rufaa ya ICC, watatoa uamuzi juu ya rufaa ya kupinga uwezo wa ICC kusikiliza kesi inayomkabili Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo.

NI/FK

© Agence Hirondelle