Justice Info

TAARIFA ZA HIVI KARIBUNI

14.12.12 - MAJUMUISHO YA WIKI - WAFUNGWA WAWILI WA ICTR WAACHIWA MAPEMA,MWENDESHA MASHITAKA WA ICC AOMBA MSAADA BARAZA LA USALAMA

Arusha, Desemba 14,2012 (FH) - Taasisi ya Kimataifa inayorithi Kazi za Mahakama za Umoja wa Mataifa (MICT),Jumanne imewaachia huru kabla ya muda wao wa adhabu kuisha, wafungwa wawili huku Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Fatou Bensouda alihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

ICTR 

Wafungwa wawili waachiwa huru mapema: Taasisi ya Kimataifa inayorithi Kazi za Mahakama za Umoja wa Mataifa (MICT),Jumanne imewaachia huru kabla ya muda wao wa adhabu kuisha, wafungwa wawili waliokuwa wanatumikia kifungo baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.Watu hao ni pamoja na meya wa zamani wa wilaya ya Gikongoro, mkoa wa Kigali Vijijini, Paul Bisengimana na kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa Interahamwe mkoani Gisenyi, Omar Sereshago. Wawili hao walikuwa wanatumikia adhabu zao nchini Mali. 

Wanne waomba hifadhi Ufaransa: Msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Roland Amoussouga ametangaza kwamba maafisa watatu wa zamani wa serikali ya Rwanda walioachiwa huru na mahakama hiyo pamoja na afisa mmoja wa jeshi la nchi hiyo, aliyemaliza kutumikia adhabu yake, wameiomba Ufaransa iwapatie viza ya muda mrefu ya kuishi nchini humo, ili waweze kuungana na familia zao zinazoishi katika nchi hiyo. 

RWANDA  

Meya wa zamani ahukumiwa kifungo cha maisha jela: Jumatano wiki hii, Mahakama Kuu nchini Rwanda, ilimhukumu meya wa zamani, Jean Pierre Sewabeza kifungo cha maishan jela baada ya kumtia hatiani kwa kuhusika kwake katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994. 

ICC  

Mahakama yaiamuru Libya kumkabidhi Abdullah al-Senussi: Jumatatu majaji wa mahakama ya ICC walitoa amri kwa serikali ya Libya kutekeleza hati ya kumkamata Abdullah al-Senoussi. Mahakama hiyo inamshitaki Mkuu huyo wa zamani wa Idara ya Usalama katika utawala wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi kwa uhalifu dhidi ya binadamu. 

Rufaa ya kupinga ICC kutosikiliza kesi ya Gbagbo yatupwa: Majaji wa Mahakama ya Rufaa ya ICC, Jumatano kwa kauli moja walitupilia mbali rufaa iliyopinga mahakama ya ICC kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi ya aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo. Hivi sasa Gbagbo anakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu mbele ya mahakama hiyo. 

Bensouda ahutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataiafa: Mwendesha Mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda Jumanne alihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York na kuliomba msaada wa kuwatia mbaroni watuhumiwa. Alisema tangu mahakama yake itoe hati za kukamtwa kwa watumiwa kwa mashitaka ya mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita dhidi ya maafisa waandamizi wanne, akiwemo mkuu wa nchi, Omar Al-Bashir, hakuna hata mmoja wao aliyeletwa mbele ya mahakama hiyo kujibu tuhuma zake. 

Kesi ya Bemba yaahirishwa hadi Machi mwakani: Majaji wa mahakama ya ICC, Alhamisi waliahirisha kusikiliza kesi ya utetezi inayomkabili Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean Pierre Bemba, anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. 

WIKI IJAYO 

ICC 

Hukumu ya Ngudjolo kutolewa wiki ijayo:  Jumanne ijayo, Desemba 18, majaji wa ICC watatoa hukumu katika kesi inayomkabili Mathieu Ngodjolo anayeshitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita kwa madai ya kushiriki kwake katika mashambulio ya Bogoro, katika wilaya ya Ituri, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Februari 24, 2003.  

ICTR 

ICTR kutoa hukumu yake ya mwisho: Alhamisi ijayo, majaji wa watotoa hukumu katika kesi ya mwisho kuwahi kusikilizwa na ICTR inayomhusu Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda, Augustin Ngirabatware. Anashitakiwa kwa kula njama za kufanya mauaji, mauaji ya kimbari au kushiriki mauaji ya kimbari,uchochezi na uhalifu dhidi ya binadamu. 

RWANDA     

Kesi ya Mugesera kuanza kuunguruma wiki ijayo: Kesi ya mwanasiasa wa zamani wa Rwanda, Leon Mugesera inatarajiwa kuanza kusikilizwa Jumatatu ijayo, Desemba 17,mbele ya Mahakama Kuu ya Rwanda. Mugesera anakabiliwa na mashitaka ya kuchochea mauaji ya kimbari kupitia hotuba aliyoitoa katika lugha ya Kinyarwanda mwaka 1992 katika mkutano wa chama chake cha siasa, Kaskazini mwa Rwanda. 

NI/FK

© Agence Hirondelle