Justice Info

TAARIFA ZA HIVI KARIBUNI

14.12.12 - MICT/CONVICTS - WAFUNGWA WAWILI WA ICTR WAACHIWA HURU MAPEMA

Arusha, Desemba 14,2012 (FH) – Taasisi ya Kimataifa inayorithi Kazi za Mahakama za Umoja wa Mataifa (MICT),Jumanne imewaachia huru kabla ya muda wao wa adhabu kuisha, watu wawili waliokuwa wanatumikia kifungo baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.

Watu hao ni pamoja na meya wa zamani wa wilaya ya Gikongoro, mkoa wa Kigali Vijijini, Paul Bisengimana na kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa Interahamwe mkoani Gisenyi, Omar Sereshago. Wawili hao walikuwa wanatumikia adhabu zao nchini Mali.

Wakati anaachiwa,Bisengimana alikuwa ameshatumikia theluthi mbili ya kifungo cha miaka 15 alichopewa.Alikuwa kizuizini tangu Desemba 4, 2001.

Meya huyo alitiwa hatiani Aprili 13, 2006 kwa kusaidia na kuunga mkono kutendeka kwa uhalifu wa kuua na kuteketeza kizazi kama uhalifu dhidi ya binadamu baada ya yeye mwenyewe kukiri makosa hayo.

Serushago kwa upande wake ameachiwa akiwa ameshatumikia robo tatu ya kifungo cha miaka 15 jela alichopewa Februari 5, 1999 baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu. Kiongozi huyo wa wanamgambo alikuwa kizuizini tangu Juni 9, 1998. Yeye pia kama alivyo mfungwa mwenzake alikiri kwa hiari yake mashitaka hayo dhidi yake.

Katika uamuzi uliomhusu Bisengimana, Rais wa MICT, Jaji Theodor Meron alisema, ‘’Baada ya kuchambua kwa makini vipengele vilivyomo katika sheria na pia mazingira maalum ya kesi ya Bisengimana, nimeonelea kwamba anastahili kuachiwa huru mapema na mara moja.’’ Alimwelekeza Msajili kuifahamisha serikali ya Mali juu ya uamuzi huo.

Uamuzi wa MICT ambayo ilianzishwa rasmi 2010 kurithi kazi za mahakama mbili za Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu katika Yogoslavia ya zamani (ICTY) imeonekana kutatua mgogoro wa kisheria wa muda mrefu kati ya mahakama hizo mbili juu ya suala hilo. 

Katika ICTR, mfungwa anatakiwa kutumikia robo tatu ya adhabu aliyopewa kabla ya kufikikiriwa kuachiwa huru mapema wakati ICTY, uamuzi kama huo unaweza kutolewa iwapo mfungwa atakuwa ameshatumikia theluthi mbili ya adhabu yake. 

Lakini katika uamuzi wake, Rais Meron alisema ‘’Nimeonelea kwamba wafungwa wote wanaosimamiwa na MICT wanastahili kutendewa sawa.’’    

NI/FK

© Hirondelle News Agency