Justice Info

TAARIFA ZA HIVI KARIBUNI

21.12.12 - MAJUMUISHO YA WIKI - ICC YAMWACHIA HURU KIONGOZI WA WANAMGAMBO,NGIRABATWARE KUTUMIKIA MIAKA 35 JELA

Arusha, Desemba 21,2012 (FH) – Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) wiki hii imemwachia huru, kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mathieu Ngudjolo huku Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), ikimhukumu kifungo cha miaka 35 jela, Waziri wa zamani wa Mipango, Augustin Ngirabatware baada ya kumtia hatiani kwa mauaji ya kimbari.

ICC 

Majaji wamwachia huru Ngudjolo: Majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Jumanne walimwachia huru kwa mashitaka yote aliyokabiliwa nayo kiongozi wa zamani wa wanamgambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Mathieu Ngudjolo. Kiongozi huyo alishitakiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu yaliyodaiwa kufanyika Mashariki mwa DRC mwaka 2003. Majaji waliamuru mshitakiwa huyo kuachiwa mara moja na kuitaka ofisi ya Msajili wa Mahakama hiyo kuchukua hatua zinazofaa za kuwalinda mashahidi.Majaji walisema kwamba kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Mahakama imeshindwa kubaini pasipo mashaka yoyote kwamba mshitakiwa alikuwa kiongozi wa kundi la wapiganaji la Lendu, lililoshiriki kwenye mapigano katika eneo la Bogoro, Mashariki mwa DRC, Februari 24, 2003. 

Marekani yataka Mudacumura,Ntaganda wakamatwe: Marekani Jumanne ilitoa wito wa kukamatwa kwa waasi wawili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Conmgo (DRC),ikiwa ni pamoja na Sylvestre Mudacumura na Bosco Ntaganda wanaotakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.Wito huo umetolewa baada ya ICC kumwachia huru kiongozi wa zamani wa wanamgambo wa DRC, Mathieu Ngudjolo.Mudacumura ni kamanda wa kundi la waasi la FDLR ambapo Ntaganda ni kiongozi wa kundi la CNDP.    

ICTR 

Ban Ki-moon ateua Msajili mpya wa ICTR: Jumatano Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alimteua Christopher Bongani Majola, kuwa Msajili mpya ICTR. Raia huyo wa Afrika Kusini ataanza kazi yake rasmi Januari Mosi, 2013 kwa muda wa miaka minne au hadi hapo ICTR itakapofungwa.Majola anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Adama Dieng kutoka Senegal, ambaye aliteuliwa na Katibu Mkuu huyo wa UN, kuwa Mshauri Maalum wa Kuzui Mauaji ya Kimbari tangu Julai 17, 2012. 

Waziri wa zamani wa mipango ahukumiwa miaka 35 jela: Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda(ICTR) imemhukumu kifungo cha mika 35 jela Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda,Augustin Ngirabatwara baada ya kumtia hatiani kwa mashitaka matatu ya mauaji ya kimbari.Mahakama iliyokuwa inaongozwa na Jaji William Sekule kwa kauli moja imemtia hatiani Ngirabatware kwa mashitaka ya mauaji ya kimbari, uchochezi na ubakaji kama uhalifu dhidi ya binadamu. Katika hukumu yake,mahakama imemtia hatiani Waziri huyo wa zamani kwa mauaji ya kimbari kutokana na ukweli kwamba alichochea, kusaidia na kuunga mkono mashambulizi na mauaji dhidi ya Watutsi katika wilaya yake ya Nyanyumba, mkoa wa Gisenyi, Kaskazini mwa Rwanda alikozaliwa.

RWANDA

Kesi ya Mugesera yaanza kusikilizwa: Kesi inayomkabili mwanasiasa mkongwe wa Rwanda, Leon Mugesera ilianza kusikilizwa rasmi Jumatatu mbele ya Mahakama Kuu mjini Kigali.Hata hivyo mawakili wake wanadai kuwa kesi hiyo iko nje ya mamlaka ya mahakama hiyo.Kesi imeahirishwa hadi Desemba 24,mwaka huu. Mugesera anashitakiwa kwa kuchochea mauaji ya kimbari katika hatuba yake aliyoitoa mwaka 1992.

Jaji wa Ufaransa akataa kuwarejesha Wanyarwanda wawili kwenda kwao: Jaji mmoja nchini Ufaransa Jumatano alikataa kuwarejesha Kigali wanyarwanda wawili ikiwa ni pamoja na Waziri wa zamani Hyacinthe Nsengiyumva Rafiki na afisa mmoja mwandamizi, Venuste Nyombayire. Wote wawili walishitakiwa kwa kushiriki kwao katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini mwao.Mahakama ya mjini Paris, Ufaransa iliamua kwamba mashitaka ya kutaka kuwarejesha makwao hayana uzito wa kutosha na inashindikana kuyahusisha moja kwa moja na watuhumiwa hao. 

NI/FK

© Agence Hirondelle