31.05.12 - ICTR/NZABONIMANA - WAZIRI WA ZAMANI WA RWANDA AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA JELA

Arusha, Mei 31, 2012 (FH) –Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) imemtia  hatiani Waziri wa zamani wa Vijana wa Rwanda, Callixte Nzabonimana kwa mashitaka manne ya mauaji ya kimbari na kumhukumu kifungo cha maisha jela.

 

Jaji Solomy Balungi Bossa kutokaUgandaaliyekuwa anaongoza jopo la majajai watatu katika kesi hiyo amesema mahakama yake imekubaliana kwa kauli moja kumtia hatiani Nzabonimana kwa mashitaka ya mauaji ya kimbari, uchochezi wa mauaji hayo, kuteketeza kizazi na kula njama za kufanya mauaji hayo katika mkoa wake wa Gitarama, katikati yaRwanda, mwaka 1994.

‘’Kwa uhalifu huu, na kwa mazingira yote muhimu katika kesi hii, Mahakama inakuhukumu wewe adhabu ya kifungo cha maisha jela,’’ alitamka Jaji Bossa huku Nzabonimana mwenyewe akiwa amesimama.

Mahakama ilibaini kwamba Aprili 18, 1994 katika mkutano kwenye ofisi za mkoa wa Gitarama alikubaliana na viongozi wenzake wa serikali ya mpito kuchocheo mauaji dhidi ya Watutsi.

Katika hukumu hiyo Nzabonimana alitiwa hatiani pia kwa mauaji ya kimbari yaliyofanyika dhidi ya Watutsi waliokuwa wanapata hifadhi katika ofisi za mkoa wa Gitarama.

Wakili wa Nzabonimana,Vincent Courcelle-Labrousse aliiambia Hirondelle muda mfupi baada ya hukumu hiyo kwamba atakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

‘’Bila shaka tutakata rufaa.Kesi ndiyo kwaanza inaanza kwenye rufaa,’’ alisema wakili huyo kutoka Ufaransa.

Waziri huyo alitiwa mbaroni nchini Tanzania Februari 18, 2008 na kesi yake ilianza Novemba 9, 2009 na kuhitimishwa Septemba 12,2011.  Mwendesha mashitaka  aliita mashahidi 20 wakati upande wa utetezi uliita mashahidi 38.

NI/FK
© Hirondelle News Agency