Justice Info

01.12.12 - ICTR/NGIRABATWARE - KESI YA MWISHO ICTR DHIDI YA WAZIRI WA ZAMANI KUTOLEWA HUKUMU DESEMBA 20

Arusha, Desemba 1,2012 (FH) – Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda(ICTR) itatoa hukumu ya kesi inayomkabili Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda,Augustin Ngirabatwara Desemba 20, 2012, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mahakama hiyo.

Hii itakuwa na kesi ya mwisho kutolewa hukumu na mahakama hiyo ya awali ya Umoja wa Mataifa. 

Iwapo kutakuwapo na kukata rufaa baada ya hukumu, rufaa hiyo itasikilizwa na Taasisi Itakayorithi Kazi za Mahakama Mbili za Umoja wa Mataifa (MICT) ikiwemo ICTR na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita Katika Yugoslavia ya zamani (ICTY).  

Wakati wa kuwasilisha hoja za mwisho Julai 23, mwaka huu, mwendesha Mashitaka aliiomba mahakama hiyo kumpatia adhabu ya kifungo cha maisha jela Waziri huyo iwapo atatiwa hatiani kwa kuhusika na mauaji hayo mwaka 1994.

Akitoa sababu kwa nini Waziri huyo apewe adhabu kali kiasi hicho, Mwendesha Mashitaka, Rashid Rashid alisema ‘’kutokana na ushahidi ulitolewa mahakamani, nia ya Ngirabatware ya kutekeleza mauaji ya kimbari imethibitishwa pasipo mashaka.’’ 

‘’Alitekeleza, kuandaa,kuchochea, kuhimiza, kusaidia na kupitisha adhma ya mauaji dhidi ya raia wa Kitutsi.Ametekeleza uhalifu huo katika wilaya alikozaliwa ya Nyamyumba, mkoa wa Gisenyi, Kaskazini mwa Rwanda,’’ mwendesha mashitaka alisema. 

Kwa upande wake, Wakili wa utetezi katika kesi hiyo , Mylene Dimitri aliiomba mahakama iliyokuwa inaongozwa na Jaji William Sekule toka Tanzania,imwachie  huru mteja wake kwa madai kwamba mwendesha mashitaka ameshindwa kuthibitisha mashitaka pasipo mashaka. 

‘’Ushahidi uliotolewa na Ngirabatware ni zaidi ya ushahidi wa kuaminika na umeonyesha zaidi ya vigezi vya kuwepo  mashaka katika kesi ya mwendesha mashitaka hivyo hamna budi kumwachia huru,’’ Wakili Dimitri aliisihi mahakama. 

Alisema mteja wake kamwe hakushiriki katika mauaji dhidi ya Watutsi na kwamba ushahidi wa utetezi uliotolewa katika kesi hiyo  ulikuwa ‘’ wenye maana, haikuegemea upande wowote na wa kuaminika kwa kiwango cha hali ya juu,’’  

Wakati wa usikilizaji wa kesi yake, Ngirabatware alitoa sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kwamba hakuwapo nyumbani kwao wakati uhalifu ulipokuwa unafanyika. Alidai kwamba kati ya Aprili 23 na Mei 23, 1994, alikuwa katika safari za kikazi katika nchi mbalimbali zikiwemo, Senegal, Gabon na Uswisi. 

Lakini mwendesha mashitaka alipingana na ushahidi huo kwa kudai kuwa katika kipindi hicho, mshitakiwa alikuwa mkoani Gisenyi, hususan ni katika wilaya yake ya Nyamyumba kushiriki katika kutenda uhalifu huo. 

Waziri huyo wa zamani anashitakiwa kwa kula njama za kufanya mauaji ya kimbari, mauaji ya kimbari au kushiriki mauaji hayo, uchochezi, kuteketeza kizazi na ubakaji kama uhalifu dhidi ya binadamu. 

NI 

© Hirondelle News Agency