15.12.11 - ICTR/NTAWUKULILYAYO - NAIBU MKUU WA MKOA APUNGUZIWA ADHABU YA KIFUNGO
Arusha, Desemba15, 2011 (FH) - Mahakama ya Rufaa ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Jumatano ilimpunguzia adhabu toka kifungo cha miaka 25 jela hadi 20, afisa mmoja mwandamizi wa zamani wa serikali ya Rwanda, Dominique Ntawukulilyayo baada ya kumtia hatiani kwa kusaidia kufanyika mauaji ya kimbari mkoani kwake mwaka 1994.
‘'Mahakama ya Rufaa inathibitisha kumtia hatiani Dominique Ntawukulilyayo kwa kuunga mkono na kusaidia kufanyika kwa mauaji ya kimbari kutokana na mauaji yaliyotendeka katika kilima cha Kabuye (mkoa wa Butare, Kusini mwa Rwanda),'' Jaji Kiongozi Carmel Agius alitamka.
Muda mfupi kabla ya hukumu hiyo, Jaji Agius alisema Ntawukulilyayo ameshinda moja ya hoja zake za rufaa ambayo alipinga yeye kutiwa hatiani kwa mauaji ya kimbari kutokana na matukio ya mauaji ya kilima cha Kabuye.
‘'Mahakama ya awali ilikosea kwa kumtia hatiani Ntawukulilyayo kwa mashitaka ya kuamuru mauaji yaliyofanyika kilima cha Kabuye na kutupilia mbali adhabu aliyopewa kwa kutiwa hatiani kwa kosa hilo,'' alisema Jaji Agius.
Ntawukulilyayo alikuwa Naibu Mkuu wa mkoa wa Gisagara, katika mkoa wa Butare.
Mahakama ya Rufaa pia imekubaliana na maamuzi ya mahakama ya awali kwamba Ntawukulilyayo aliwashawishi wakimbizi wa Kitutsi eneo la soko la Gisagara kwenda kupata hifadhi katika kilima cha Kabuye.
‘'Ntawukulilyayo alijua kwamba wakimbizi wa Kitutsi hawatalindwa katika kilima hicho cha Kabuye na badala yake watauawa,'' hukumu hiyo ilifafanua.
Mahakama ya Rufaa pia haikushawishiwa na hoja ya mrufani kwamba adhabu ya kifungo cha miaka 25 aliyopewa awali ni kali mno kulinganisha na tuhuma alizotiwa nazo hatiani na hivyo kumpunguzia adhabu hadi kifungo cha miaka 20 jela hususa ni baada ya kufutiwa kosa la mauaji ya kimbari katika kilima cha Kabuye.
Ntawukulilyayo alitiwa mbaroni nchini Ufaransa mwaka 2007 na kuhamishiwa makao makuu ya ICTR Juni 5, 2008 kujibu tuhuma dhidi yake.
Alizaliwa mwaka 1942 wilayani Mubuga, mkoa wa Gikongoro, Kusini mwa Rwanda.
Kesi yake ilianza kusikilizwa Mei 6, 2009. Mwendesha mashitaka aliita mashahidi 12 wakati upande wa utetezi nao uliwasilisha mahakamani mashahidi 23 akiwemo Ntawukulilyayo mwenyewe.
NI
© Hirondelle News Agency


