23.03.12 - WIKI IJAYO - MAHAKAMA KUFANYA MIKUTANO KATIKA KESI ZA BEMBA NA NGIRABATWARE JUMANNE
Arusha, Machi 23,2012 (FH) – Kesi inayomkabili kiongozi wa kundi la waasi la zamani la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ,Jean Pierre Bemba mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu(ICC) na ile inayomkabili Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda , Augustin Ngirabatware mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) zitakuwa na mikutano tofauti Jumanne ijayo kuamua namna ya kuendelea na kesi hizo.
ICC
Kesi ya Bemba: Jumanne ijayo Machi 27, majaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) watakutana na pande mbili zinazohusika katika kesi hiyo ili kuamua namna ya kuendelea na usikilizaji wa kesi hiyo baada ya upande wa mwendesha mashitaka kukamilisha kuita mashahidi wake 40 kuunga mkono mashitaka dhidi ya mshitakiwa.Kwa mujibu wa sheria na taratibu za mahakama hiyo wawakilishi wa walioathiriwa na uhalifu uliofanywa wanaweza kupewa nafasi ya kuwasilisha mashahidi kabla ya upande wa utetezi kuita mashahidi wake. Bemba, Seneta wa zamani waCongona Kiongozi wa kundi la waasi la MLC, anakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita aliodaiwa kufanya katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kati ya mwaka 2002 na 2003.
ICTR
Kesi ya Ngirabatware: Mwendesha mashitaka katika kesi ya Waziri wa zamani wa Mipango wa Rwanda, Augustin Ngirabatware anatarajiwa Jumanne ijayo Machi 27, kuijulisha mahakama katika kikao cha pamoja lini mashahidi wake wawili wa ziada waliobakia wataweza kutoa ushahidi wao wa kupinga uwepo wa mtuhumiwa huyo nchini Rwanda kati ya Aprili 23 na Mei 23, 1994. Tayari mashahidi sita kati ya wanane wa ziada wameshatoa ushahidi wao mbele ya mahakama hiyo. Mshitakiwa anadai kwamba katika kipindi hicho alikuwa katika ziara ya kikazi katika nchi zaSenegalnaSwazilandna hivyo asingeweza kushiriki katika uhalifu anaodaiwa kufanya. Waziri huyo wa zamani anashitakiwa kwa mauaji ya kimbari, kula njama za kufanya mauaji hayo, kushiriki katika mauaji hayo, uchochezi , kuteketeza kizazi na ubakajikamauhalifu dhidi ya binadamu.
NI/SM/FK
© Hirondelle News Agency
