15.09.11 - ICTR/MWENDESHA MASHITAKA - JALLOW ATEULIWA TENA KUENDELEA NA WADHIFA WAKE ICTR

Arusha, Septemba 15, 2011 (FH) - Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Jumatano limemteua tena Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Hassan Bubacar Jallow kuendelea na wadhifa huo kwa kipindi kingine cha miaka mitatu.

Taarifa iliyotolewa na Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa kwenye mtandao Alhamisi imeeleza kwamba kwa kutekeleza azimio namba 2006 la mwaka 2011, ambalo lilikubaliwa bila kupingwa, Baraza hilo limemteua tena Jallow, raia wa Gambia, kwa mkata mwingine wa kazi kuanzia Septemba 15, 2011 na kuendelea hadi Desemba 31, 2014.

‘'Baraza limezingatia taratibu za Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa kwa kuongeza mkataba wa ajira wa Jallow ambao ulikuwa unaisha Desemba 31, 2011, kwa kipindi kingine cha miaka mitatu. Baraza limezingatia pia uamuzi huo wa sasa kutokana na uamuzi wa awali wa Baraza la Usalama juu ya kuhitimisha kazi za mahakama hiyo,'' inasomeka sehemu ya uamuzi huo.

Baraza pia limeitaka ICTR kuchukua hatua zote zinazowezekana kuhitimisha haraka kazi yote inayobakia katika mahakama hiyo, kabla ya Desemba 31,2014.

Kesi sita bado ziko mbele ya Mahakama hiyo zikiwa katika hatua mbalimbali, ikiwemo moja inayohusisha mawaziri wanne wa zamani wa Rwanda ambayo hukumu yake inatarajiwa kutolewa Septemba 30, mwaka huu. Kesi moja inasubiri kuanza kusikilizwa huku nyingine moja ipo katika hatua ya rufaa kufuatia uamuzi wa kuihamishia kusikilizwa nchini Rwanda.

Pia zipo kesi 10 zenye jumla ya watuhumiwa 19 ambazo zipo katika hatua mbalimbali za rufaa. Mbili zimepangwa kusikilizwa Septemba 26 na 27, mwaka huu wakati nyingine mbili zimepangiwa kutolewa hukumu Septemba 28, mwaka huu pia.

Jallow aliteuliwa kwa mara ya kwanza kushika wadhifa Mwendesha Mashitaka wa ICTR Septemba 4, 2003, akiziba nafasi iliyoachwa na Mswisi, Carla Del Ponte ambaye alikuwa Mwendesha Mshita wa ICTR na Mahakama nyingine ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita katika Yogoslavia ya zamani (ICTY) tangu Septemba 1999.

Aliwahi kushika wadhifa wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Gambia, Waziri wa Sheria wan chi hiyo kati ya 1984 na 1994 na baadaye kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Gambia. Mwaka 1998 aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa Mtaalamu wa Kimataifa wa Masuala ya Sheria na kufanya tathmini ya kimahakama ya za ICTR and ICTRY.

Jallow pia alifanyakazi kama Mtalaamu wa Sheria kwa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na sasa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Madola na pia aliufanyia kazi mswaada wa Kimataifa wa Haki za Binadamu na Raia wa Afrika alioridhiwa mwaka 1980.

NI/FK

© Hirondelle News Agency