25.05.04 - ICTR/ECONOMY - MAKALA/KUFUNGWA KWA ICTR KULETA KITIMTIM KWA WAKAZI WA ARUSHA
Na Nicodemus Ikonko wa Hirondelle-Arusha
Arusha, Mei 25, 2004 (FH)- Bado miaka mitano tu kuanzia sasa Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) itahitimisha majukumu yake mjini Arusha, nchini Tanzania. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoanzisha Mahakama hiyo ili kushughulikia watuhumiwa wa mauaji hayo, imeshaamua kwamba mahakama hiyo itafunga shughuli zake ifikapo mwaka 2008.
Tayari ICTR yenyewe imeshapanga mikakati ya kuhakikisha kwamba inatimiza majukumu yake ifikapo mwaka huo wa 2008. Kamati ya watu sita imeshaundwa ili kutathmini ni namna gani kesi ambazo hazitakuwa zimekamilka ifikapo mwaka huo, zihamishiwe kwenye Mahakama za nchi wanachama ikiwemo Rwanda ili zikaendelee kusikilizwa katika nchi hizo.
Ingawa tukio la hivi karibuni la Jaji wa mahakama hiyo , Andresia Vaz kujitoa katika kusikiliza moja ya kesi na hivyo kuchelewesha mwendendo wa kesi hiyo, kasi ya usikilizaji wa kesi mbalimbali katika mahakama hiyo ni ya kuridhisha. Kesi tatu zinaweza kusikilizwa kila siku kwa wakati mmoja katika vyumba vitatu tofauti vya mahamakama hiyo na wakati mwingine mahakama moja inaweza kusikiliza kesi mbili kwa siku, moja asubuhi na nyingine mchana.
Hivi sasa kesi sita zinazojumuisha watuhumiwa 20 zinaendelea kusikilizwa katika hatua mbalimbali ambapo pia inatarajiwa kuwa ifikapo Juni mwaka huu mahakama hiyo itatoa hukumu za kesi mbili ambazo tayari zimeshakamilika katika hatua ya kusikilizwa. Mapema mwezi huu, Umoja wa Ulaya(EU) umekubali kufadhili miradi minane ya mahakama hiyo yenye thamani ya fedha za Ulaya milioni 1.5 (sawa na shilingi bilioni 1.5 za Tanzania). Fedha hizo zimetolewa ili kuhakikisha kwamba mahakama hiyo inakamilisha majukumu yake kama ilivyokwishakuamuliwa na Baraza la Usalama.
Inaelekea kila kitu kimeshaandaliwa tayari kabisa kwa kufungwa kwa shughuli za mahakama hiyo hapa Arusha ifikapo mwaka 2008. Lakini swali moja la muhimu sana kujiuliza ni kwamba je wananchi wa Arusha iliko mahakama hiyo wanaelewa kwamba kufungwa kwa shughuli za mahakama hiyo kutaleta athari gani kijamii na kiuchumi ?
Kwa mujibu wa Chama cha wafanyakazi wa ICTR, mahakama hiyo ina jumla ya wafanyakazi 668 kutoka nchi 87 duniani. Kati ya hao 231 ambao ni zaidi ya asilimia 30 ni watanzania. Kwa ujumla wao wafanyakazi wote wa mahakama hiyo wanahodhi magari binafsi zaidi ya 600 na kila mmoja wao ameajiri wenyeji kati ya mmoja hadi wanne kwenye kazi kama vile mtumishi wa ndani, mtunza bustani, dereva na mlinzi. Chama cha wafanyakazi wa mahakama hiyo pia kina mradi wa mgahawa ambao umeajiri watanzania wengine 25.
‘’ Hatutaki kujifagilia sisi wenyewe lakini kila mmoja wetu ameleta tofauti kubwa katika maisha ya watu wanaotunzunguka hapa,’’ alisema Phillis Grobl, Rais wa mstaafu wa chama cha wafanyakazi wa ICTR.
Alisema licha ya watanzania ambao wananufaika moja kwa moja na ajira toka kwa wafanyakazi wa ICTR, jamii ya wafanyabiashara wa mjini Arusha pia wanafaidika vilivyo kutokana na kuwepo kwa mahakama hiyo. Akitoa mifano aliyataja baadhi ya makampuni yanayofaidika kuwa ni pamoja na vituo vya petroli, wakala wa bima, huduma za posta na simu, makampuni ya simu za mikononi, makampuni ya utalii na usafirishaji, maduka mbalimbali makubwa ya wageni na wenyeji, mabenki, shule zile za kimataifa na nyingine zinazotumia Kiingezea kama lugha kuu ya kufundishia na makampuni ya huduma muhimu kama vile maji na umeme.
Lakini Grobl alionya na kudokeza pia kwamba makampuni yenye nyumba za kupanga ‘’ yataporomoka kabisa ifikapo 2008’’. Karibu asilimia 75 ya maafisa waandamizi wa mahakama hiyo hulipa kodi ya pango kati ya dola 800 na 1,500 kwa mwezi (kati ya shilingi laki 8 na milioni 1.5 za Tanzania). Pamoja na malipo hayo ya nyumba, ICTR imekodi asilimia zaidi ya 70 ya ofisi za Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC).
‘’ Bila shaka malipo ya pango la ofisi yatashuka kwa sababu hakuna mtanzania atakayeweza kulipa kodi ya pango la ofisi kati ya dola 500 na 1,200 kila mwezi (shilingi laki 5 na milioni 1.2 za Tanzania),’’ Meneja wa Nyumba wa AICC, Francis Kulwa aliiambia Hirondelle katika mahojiano.
Licha ya kupangisha ofisi, AICC pia inawakodishia nyumba zake kadhaa wafanyakazi wa ICTR. Kwa ujumla wake huduma hizo mbili Kulwa amesema zinaipatia AICC jumla ya dola za Kimarekani milioni 1.2 sawa na shilingi bilioni 1.2 za Tanzania kwa mwaka.
Alipoulizwa ni jinsi gani AICC itaweza kuziba pengo hilo pindi mpangaji huyo ICTR atakapoondoka, kulwa alisema ‘’ asilimia ipatayo 30 ya wateja wetu hasa wale wanaojali ubora wa ofisi na huduma zetu watarejea kupanga tena AICC na wale ambao bado wapo nasi mpaka sasa kama vile Pride Tanzania na Hoteli ya Serena wanahakikishiwa kubaki.’’
Wakati mahakama hiyo ilipokuwa inaanzishwa mjini Arusha mwishoni mwa mwaka 1995, zaidi ya wapangaji 100 walilazimika kuondoka kwenda kupanga sehemu nyingine nje ya AICC ili kutoa nafasi ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo.
Hali hiyo ya uwezekano wa kuyumba kwa uchumi wa Arusha baada ya ICTR kufunga kazi yake hapa pia inamtia wasiwasi, Simom Mapolu, Mshauri wa Masuala ya Menejimenti mjini Arusha. ‘’ Uendelezaji wa miradi ya nyumba za kupanga uko gizani,’’ alisema. Alitoa mfano wa nyumba zinazomilikiwa na Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF) mjini Arusha ambazo hivi sasa asilimia 70 ya wapangaji wake ni wafanyakazi wa ICTR.
‘’ Kama hawataweza kutafuta miradi mbadala, nyumba hizo za PPF zitabakia tupu pindi ICTR itakapofunga shughuli zake,’’ alionya Mapolu.
Wasiwasi wa Mapolu pia unawagusa vijana wa kike na wa kiume ambao wameacha ajira serikalni katika umri wa miaka 30 na 40 ili kujiunga na ICTR. Alisema mishahara yao imepanda ghafla kutoka wastani wa shilingi 80 kwa mwezi hadi kati ya 300,000 na 400,000 kwa mwezi. ‘’ Watafanya nini baada ya ICTR kufungwa ?,’’ aliuliza na kuongeza ‘’ sidhani kama watarejea kuajiriwa tena serikalini.’’
Alisema wanahitaji kuandaliwa kisaikolojia ili kuingia katika biashara ndogondogo au kwenda kusoma masomo ya juu.
‘’ Wananchi wa Arusha na jamii ya wafanyabiashara wanapaswa kufahamu kwamba ICTR siyo taasisi ya kudumu nchini Tanzania hivyo chochote wanachovuna kutokana na kuwepo kwa mahakama hiyo lazima wakifanye kiwe endelevu,’’ alionya Niarira Magunda, Afisa Biashara wa Manispaa ya Arusha.
Magunda amesema ICTR imeleta chachu ya mabadiliko mbalimbali ya maisha mjini Arusha katika nyanja za biashara na huduma. Uwezo wa manunuzi umeongezeka, mahitaji ya nyumba yamepanda na ajira zimepanuka.
Alisema hayo yote ukichanganya na uwezo mkubwa wa kifedha wa wafanyakazi wa ICTR bila shaka utaathiri biashara na huduma pindi mahakama hiyo itakapofungwa.
Lakini Rais mstaafu wa wafanyakazi wa ICTR anawafariji wakazi wa Arusha kwa kusema kuwa angalau kila mmoja anajua kwamba mahakama hiyo siku moja lazima itafikia mwisho wake. Alisema bila shaka uzoefu na ujuzi mkubwa walioupata watanzania waliobahatika kufanyakazi ICTR utawawezesha kutafuta mbinu nyingine ya kuishi au kupata ajira nyingine kwa manufaa ya jamii ya Arusha na nchi kwa ujumla wake.
NI/FH(ICTR’’0525s)


