12.11.04 - ICTR/DEFENCE - WATAKA JALADA LA WAKILI MWENZAO ALIYEFUKUZWA LICHUNGUZWE UPYA

Arusha, November 11th, 2004 (FH)- Chama cha Mawakili wanaofanya kazi katika Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Halaiki ya Rwanda(ADAD) kinataka jalada la mwenzao aliyefukuzwa kazi wiki mbili zilizopita lichunguzwe upya.

Msajili wa ICTR alimfukuza kazi wakili Jean Yaovi Degli kwa tuhuma za kuiibia Mahakama dola za kimarekani laki tatu kwa kushirikiana na msaidizi wake.

Katika taarifa iliyopokelewa na Shirika la Habari la Hirondelle siku ya Jumatatu wiki hii ADAD ilipendekeza, “utaratibu unaofuatwa hivi sasa uachwe ”, kwa sababu wamedai unadhihirisha kuwa na matatizo mengi. Mawakili hao wa utetezi, waliomba kwamba, “uchunguzi mpya ufanyike na chombo huru kisichopendelea upande wowote”. Chama hicho kilipendekeza pia kwamba iwapo chama cha wanasheria mjini Paris, Ufaransa hakitashughulikia suala hilo basi , Degli anapaswa kufika mbele ya baraza maalumu na huru litakaloweza kusikiliza suala lake. ADAD vilevile, walisikitishwa na hali ya mwenzao aliyetimuliwa, “kutokupewa notisi wala nafasi ya kujitetea dhidi ya uamuzi wa msajili.” Vilevile chama hicho kilihoji hali ya kutoa uamuzi wa haraka kumfukuza kazi wakili Degli kabla ya kuthibitika kwa madai. Huku wakifahamu uzito wa tuhuma zilizopo dhidi ya Degli, mawakili wenzake walisema iwapo tuhuma hizo zitabainika kuwa ni za kweli , “ADAD italaani vikali.”

Jean Yaovi Degli alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha ADAD na wakili kiongozi wa Brigadier Gratien Kabiligi ambaye anatuhumiwa kushiriki mauaji ya halaiki. ADAD “wameomba” kwamba katika hali iliyojitokeza, “haki za mtuhumiwa zipewe kipau mbele.”

SV/NI/GA/AT/FH (DEF’’1111s)