08.12.04 - ICTR/DEFENCE - MAWAKILI WAOMBA KUSIKILIZWA KATIKA KESI YA BAGOSORA NA WENZAKE
Arusha, Desemba 8, 2004 (FH) – Chama cha Mawakili Wanaofanyakazi Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), ADAD kimeomba kutoa hoja zao mahakamani hapo kama ‘’marafiki wa mahakama’’ katika kesi ya mauaji ya kimbari dhidi ya kundi la kwanza la maafisa wanne waandamizi wa zamani wa jeshi la Rwanda.
Katika maombi yao waliyowakilisha mahakamani Novemba 30,mwaka huu, ADAD imeomba kwamba hatua ya kumfukuza kazi mmoja wa mawakili katika kesi hiyo isitishwe hadi mwishoni mwa kesi hiyo.
Msajiliwa ICTR, alimtimua kazi wakili, Jean Yaovi Degli kutoka Togo kwa tuhuma za kujipatia fedha za ICTR kwa njia ya udanganyifu. Alikuwa ni wakili kiongozi wa mtuhumiwa Brigadia Jenerali wa zamani wa jeshi la Rwanda, Gratien Kabiligi, mmoja wa watuhumiwa wanne katika kesi hiyo.
Uamuzi wa kumtimua Degli umekuja wakati mbaya zaidi ambapo upande wa mwendesha mashtaka ukiwa umeshahitimisha kuwasilisha mahakamani mashahidi wao wote. Kabiligi ametoa hoja kwa majaji kwamba iwapo uamuzi wa kumfukuza kazi wakili wake hautabadilishwa, kesi yake ‘’ itapata athari ya kupoteza haki zake ambazo hazitaweza kurekebishwa hapo baadaye.’’
‘’ Wakili wangu anaifahamu vizuri kesi yangu zaidi ya yeyote katika mkakati wetu wa utetetezi. Tumepanga mikakati hiyo pamoja na kuifuatilia kwa makini,’’ alidai Kabiligi.
Watuhumiwa wengine watatu waliosalia nao wamedai ‘’kuna uwezekano wa kuathiriwa pia’’ kufuatia uamuzi huo. Wamedai kwamba Degli katika kipindi fulani kijacho angekuwa anawahoji mashahidi wanaoogusa watuhumiwa wote wanne wakati upande wa mwendesha mashtaka atakapoanza kuwasilisha mashahidi wake mahakamani hapo Januari, mwakani.
ADAD inadai kwamba ni kutokana na kuunga mkono hoja hizo za Kabiligi na watuhumiwa wenzake ndicho kilichowasukuma kuomba kuwasilisha hoja zao kama marafiki wa mahakama.
Wameiomba mahakama kutoa uamuzi wa kisheria juu ya hatua ya kumtimua kazi Degli na wakati uliotumika katika kufikia uamuzi huo.
ADAD pia inadai kwamba Msajili wa ICTR amekiuka haki ya mtuhumiwa kupewa nafasi sawa ya kujitetea dhidi ya kesi inayomkabili. Sambamba na hoja hizo, ADAD imeongeza kwamba uamuzi wa kumfukuza kazi wakili huyo utachelewesha usikilizaji wa kesi hiyo na unapingana na juhudi zinazofanyika za kuhitimisha kazi za mahakama hii ifikapo mwaka 2008.
Pamoja na watuhumiwa wengine, Brigadia Kabiligi anashtakiwa katika kesi moja na Kanali Theoneste Bagosora, aliyekuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Ulinzi wakati wa mauaji ya halaiki.
NI/FH/(DF’’128s)
___


