08.10.09 - ICTR/HATEGEKIMANA - HATEGEKIMANA HATAPANDA KIZIMBANI KUJITETEA MWENYEWE

Arusha, 08 Oktoba , 2009 (FH) - Tofauti na watuhumiwa wengine wa mauaji ya kimbari ambao mwishoni mwa kesi zao hujitetea wenyewe, afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda, Luteni Ildephonse Hategekimana hakufanya hivyo na badala yake alihitimisha kuleta mashahidi wake Jumanne wiki hii mbele ya Mahakama ya Umoja wa Mataifa.

Ahlonko Dovi toka Togo, Wakili kiongozi wa mtuhumiwa huyo, aliliambia jopo la majaji watatu wa mahakama namba II inayoongozwa na Jaji Arlette Ramaroson kutoka Madagascar, kwamba timu yake ya utetezi imetosheka na idadi ya mashahidi waliowaita na hivyo mteja wake, Hategekimana hatapanda kizimbani.

Mwendesha mashtaka ilihitimisha kesi yake Mei 4, baada ya kuita mashahidi 20 huku upande wa utetezi ulifanya hivyo pia baada ya kuleta idadi kama hiyo ya mashahidi kuunga mkono hoja zake.

Mahakama baadaye aliamuru kwamba upande wa mwendesha mashtaka uwe umewasilisha hoja zake za mwisho za utetezi kwa maandishi ifikapo Desemba 7, mwaka huu na kuutaka upande wa utetezi kufanya hivyo pia ifikapo Januari 15, 2010.

Jaji Ramaroson aliamua pia kwamba mwishoni mwa Februari mwaka ujao itakuwa ni kipindi cha pande zote mbili kutoa hoja zao za mwisho mahakamani katika tarehe itakayopangwa baadaye.

Katika maauzi yake pia, Jaji huyo alipanga kipindi cha kati ya Novemba 2 na 6, mwaka huu pande zote zinazohusika katika kesi hiyo zitakwenda nchini Rwanda kukagua maeneo kulikodaiwa kuwa uhalifu wa mauaji ya kimbari ulifanyika.

Lt. Hategekimana ni miongoni mwa watuhumiwa watano ambao Mwendesha Mashtaka  wa ICTR, Hassan Jallow alijitahidi bila mafanikio kutaka kupeleka kesi zao kwenda kusikilizwa nchini Rwanda.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Machi 16, mwaka huu.

NI

© Hirondelle News Agency