12.05.06 - ICTR/FINANCES - GHARAMA ZA ICTR KUFIKIA DOLA BILIONI MOJA IFIKAPO 2007
Arusha, Mei 10, 2006 (FH) - Msemaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda, (ICTR) ametoa waraka kwa shirika la Habari la Hirondelle hapa kwamba gharama za kuendesha mahakama hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995 hadi itakapofika 2007 zitafikia dola za Marekani bilioni moja, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 1,000 za Tanzania.
Mahakama hiyo ina makao yake makuu katika jijini Arusha, Kaskazini mwa Tanzania na ina jumla ya wafanyakazi wapatao 1,000 waliogawanywa katika idara makubwa tatu ikiwa ni pamoja na mahakama yenyewe, ofisi ya mwendesha mashtaka na ofisi ya Msajili.
Wafanyakazi hao wametoka katika nchi 85 tofauti duniani ambao idadi kubwa kati yao hufanyakazi makao makuu ya mahakama hiyo jijini Arusha.
Maafisa wanaofanyakazi katika timu za mawakili wa utetezi ambao hawana hadhi ya kuwa sehemu ya maafisa wa Umoja wa Mataifa pia wanalipwa na mahakama hii ikiwa ni sehemu ya msaada wa sheria kwa watuhumiwa wote.
Bajeti hiyo hupatikana kwa michango kutoka kwa nchi wanachama wa UN. Kwa mwaka 2006 hadi 2007 gharana zake zinakadiriwa kufikia dola milioni 250.5 sawa na shilingi bilioni zaidi 250.5 za Tanzania.Bajeti kwa mwaka uliopita ilikuwa dola milioni 230.5 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 230.5.
ICTR ilianzishwa kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la UN namba 955 lililopitishwa Novemba 8, 1994. Kesi ya kwanza kusikilizwa ilianza Januari, 1997.
Tangu wakati huo kesi za watuhumiwa 27 zimekwishahitimishwa na kutolewa hukumu.Miongoni waliotiwa hatiani ni pamoja na Waziri Mkuu wa serikali ya mpito wakati wa mauaji hayo ya mwaka 1994, Jean Kambanda ambaye sas anatumikia kifungo cha maisha jela.
Serikali ya Rwanda imeonelea kwamba mafanikio hayo ya mahakama hii hayatoshi kabisa ukilinganisha na kiwango cha bajeti kinachotolewa kwa mahakama hiyo.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Kigali, Rais wa Rwanda, Paul Kagame aliishutumu mahakama hiyo kwa kugharimu dola za Marekani bilioni 1.5 sawa na shilingi bilioni 1,500 za Tanzania kutoa hukumu kwa watuhumiwa «chini ya 40» katika kipindi cha miaka «ipatayo 11.»
Tangu kuanzishwa kwake, ICTR imeshawatia mbaroni jumla ya watuhumiwa 72 wa mauaji ya kimbari. Kati ya hao, 27 walitiwa hatiania na kupewa adhabu za vifungo mbalimbali kuanzia miaka sita jela na adhabu ya juu kabisa ya kifungo cha maisha jela ambayo walipewa wafungwa 16.
Mahakama kwa sasa inafanya uchunguzi wa kesi nyingine 27 za watuhumiwa ambapo watuhumiwa wengine 15 wanasubiri kuanza kusikilizwa kwa kesi zao.
ER/PB/MG/NI


