22.05.06 - ICTR/BAGAMBIKI/NTAGERURA - SIKU 100 BAADA YA KUACHIWA HURU BADO HAWAJAPATA NCHI YA KUWAPO

Arusha, Mei 19, 2006 (FH) - Maafisa wawili waandamizi wa zamani wa serikali ya Rwanda ambao walithibitishwa na mahakama hii kwamba hawana hatia ya mauaji ya kimbari Februari 8, mwaka huu bado hawajapata nchi ya kuwapokea ikiwa sasa ni zaidi ya siku 100 tangu kutolewa kwa thibitisho hilo.

Watu hao, Andre Ntagerura, aliyekuwa Waziri wa Usafirisha na Mawasiliano na Mkuu wa zamani wa mkoa wa Cyangugu, Kusini Magharibi ya Rwanda, Emmanuel Bagambiki, Jumatano wiki hii walitembelea ofisi ya Msajili wa Mahakama hapa kujaribu kuona uwezekano wa kupatikana kwa nchi itakayokubali kuwapokea.

Huku wakiwa wamesindikizwa na polisi wawili mmoja akiwa mtanzania na mwingine wa Umoja wa mataifa, waliiambia Hirondelle kwamba walimwomba Msajili awasaidie kuwapatia nchi ambayo watahakikishiwa “usalama” wa maisha yao na ambayo watakubalika kuishi bila matatizo.

Tangu waachiwe huru Mahakama hii imekuwa ikiwapatia hifadhi katika nyumba “maalum yenye usalama” jijini Arusha na wamekuwa wakiitwa mara kwa mara na uongozi wa mahakama kujadili hali ya upatikanaji wa nchi ya kuwapokea raia hao wa Rwanda ambao sasa wako huru.

Kwa mujibu wa vyanzo vyetu bvya habari Ntegerura na Bagambiki bado wanapenda kwenda kuishi Ufaransa au Canada lakini serikali za nchi hizo hazijatoa majibu ya maombi yao.

Pamoja na sababu nyingine inasadikiwa kwamba iwapo watakubaliwa kuchukuliwa na nchi hizo, watu hao watakuwa na uhakika wa kupewa posho ya kujikimu kila mwezi tofauti na nchi za Afrika ambazo posho ya aina hii ni nadra kutolewa au hazipo kabisa.

Kwa upande wake kwa siku za hivi karibuni Bagambiki ameshtakiwa na serikali ya Rwanda kwa tuhuma za ubakaji.

Alipoulizwa juu ya hati ya kukamatwa iliyotolewa na Rwanda baada kuonekana kuwa hana hatia kwa tuhuma za mauaji ya kimbari, Bagambiki alikiri kwamba alielezwa juu ya mashtaka hayo alipotembelea mahakama wiki hii lakini alisema hati hiyo hajaipata.

Msemaji wa mahakama hii, Tim Gallimore aliwaambia waandishi wa habari hapa Jumatano wiki hii kwamba mahakama imepokea hati ya kukamatwa Bagambiki kutoka kwa serikali ya Rwanda lakini hakufafanua kuwa mahakama hiyo itachukua hatua gani juu suala hilo.

Alipokuwa anaulizwa maswali mfululizo na waandishi wa habari juu ya hatma ya watu hao wawili alijibu kuwa “wako huru” lakini hakuonyesha kwamba zimeshapatikana nchi za kuwapokea.

PB/MG/NI