20.01.06 - ICTR/KARERA - SHAHIDI ADAI KARERA ALIPOKEA NA KUGAWA SILAHA KUULIA WATUTSI
Arusha, Januari 18, 2006(FH)-Shahidi mmoja wa upande wa mashtaka ameimbia Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) kwamba mkuu wa zamani wa mkoa wa Kigali Vijijini, François Karera, alipokea silaha Aprili 1994 zilizotumika kwa mauaji ya watu wa kabila la Kitutsi katika tarafa kadhaa zilizoko mkoani humo.
Shahidi huyo wa tano kutoka wilaya ya Nyarugenge alisema Karera alifuatana na yeye pamoja na viongozi wenzake kupokea bunduki na risasi katika wizara ya Ulinzi mjini Kigali, Aprili 16.
Akitoa ushahidi kwa jina bandia la BLX kwa sababu ya usalama wake, alisema kuwa Karera alikuwa ni mwamuzi wa pekee wa kuamua nani angepokea silaha walipokuwa wizara ya ulinzi.
«Karera alichukua silaha za kupelekwa tarafa ya ya Gitega na akasema anaenda kugawa silaha hizo mwenyewe kwa sababu wanamgambo wa Interahamwe katika wilaya hiyo hawana silaha,» BLX alidai.
Akiongozwa kutoa ushahidi wake na mwendesha mashtaka Peter Tafah kutoka Cameroon, shahidi huyo aliongeza kuwa Karera alisema kwamba ni wanachama wa chama kilichokuwa madarakani cha MRND tu ambao wangepata silaha hizo.
BLX alipokea bunduki tano wakati huo na risasi ambazo aliwagawia wanamgambo wa Interahamwe baadaye na kuzitumia kuwaua Watutsi.
«Kutoka Aprili 7, tulikuwa tunagawa silaha zilizotumika kuwaua Watutsi.Ilibidi tuzitumie kuwamaliza maadui zetu,» shahidi alisema. . Kulingana na shahidi huyo, uamuzi ulikuwa umechukuliwa katika kikao Aprili 10 uliongozwa na Mkuu wa mkoa wa Kigali mjini Tharcisse Renzaho kuwa wanachama wote wa MRND walitakiwa kupigana na Watutsi kwa kutumia kila mbinu kwa sababu walikuwa wamemwua Rais Juvenal Habyarimana ambaye ndege yake ilitunguliwa jioni ya Aprili 6.
Karera aliyeongea kwenye kikao hicho alitaka wanachama wa MRND kupigana na maadui kwa kutumia nguvu zote .Wakati wa kikao hicho Watutsi walitambulishwa kama adui.
Karera anatuhumiwa kuongoza katika mauaji ya Watutsi mkoa wa Kigali Vijijini na Mjini alipokuwa akiishi.
Anakabiliwa na mashtaka manne ya mauaji ya kimbari na ukatili dhidi ya ubinadamu.
Kesi yake ilianza kusikilizwa Januari 9 2006.
PJ/NI


