07.02.06 - ICTR/KARERA - MWENDESHA MASHTAKA AHITIMISHA KESI DHIDI YA KARERA
Arusha, Februari 3, 2006 (FH) - Mwendesha mashtaka katika kesi inayomkabili mkuu wa zamani wa mkoa wa Kigali Vijijini, François Karera, amehitimisha kesi yake Alhamisi wiki hii katika Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) baada ya kuita mashahidi 18 kuunga mkono mashtaka yake dhidi za mtuhumiwa.
Kesi hiyo imesikilizwa kwa muda mfupi tu wa siku 16 kuanzia Januari 9, mwaka huu.
Mwendesha mashtaka Charles Adeogun-Phillips wa Nigeria hata hivyo aliiambia mahakama kwamba kuna uwezekano wa kumwita mahakamani mtaalamu wa masuala ya kijamii toka Ufaransa, Andre Guichaoua kuja kutoa ushahidi wa kitalaamu.
Kesi itaendelea kusikilizwa tena Mei mwaka huu wakati mawakili wa utetezi watakapoanza kuita mashahidi wao. Tarehe kamili itatangazwa hapo baadaye.
Wengi wa mashahidi wa upande wa mashtaka walisimulia jinsi Karera alivyoongoza mauaji dhidi ya wakimbizi wa Kitutsi waliokuwa wanapata hifadhi katika kanisa katoliki la Ntarama lililopo umbali wa kilomita 30, Kusini mwa jiji la Kigali.
Walidai kwamba Karera aliwaongoza askari waliokuwa na silaha za moto pamoja na wanamgambo wa Interahamwe katikati ya Aprili 1994 kufanya mauaji dhidi ya Watutsi.
Kwa mujibu wa mashahidi hao watu wengi walipoteza maisha yao ingawaje hawakuweza kutaja idadi kamili.
Wengine walidai kuwa walikuwa mamia na wengine wakadai kwamba walikuwa maelfu ya watu walifariki. Mashahidi wengine walimhusisha Karera na mauaji yaliyofanyika wilayani Rushashi.
Mashahidi wengine wawili walidai kwamba Karera alihusika na mauaji ya diwani wa kata ya Kimisange, mkoa wa Kigali Vijijini aliyetambuliwa kwa jina la Theoneste Gakuru. Gakuru inadaiwa aliuawa baada ya kutiwa mbaroni kwa amri iliyotolewa na Karera.
Mwendesha mashtaka anamtuhumu Karera pia kwa kusababisha watu kadhaa akiwemo Gakuru kupoteza maisha yao kwa sababau ya matendo yake au kwa kutochukua hatua yeyote kuzuia mauaji hayo.
Karera anakabiliwa na mashtaka manne ya mauaji ya kimbari na ukatili dhidi ya binadamu.
PJ/NI


