14.08.12 - ICC/BEMBA - JENERALI WA UFARANSA UTOA USHAHIDI WA KITAALAMU KATIKA KESI YA BEMBA

Arusha, Agosti 14, 2012 (FH) – Shahidi wa kwanza wa utetezi katika kesi inayomkabli Jean Pierre Bemba mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) alisimama kizimbani Jumanne kama mtaalamu wa Kijeshi.

Jenerali mstaafu wa Ufaransa, Jacques Seara aliiambia mahakama hiyo kwamba ingekuwa vigumu kuwa na watoa amri za kijeshi tofauti wakati wa mgogoro. 

Bemba,Kamanda wa zamani wa kundi la waasi la MLC, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu(mauaji na ubakaji) na uhalifu wa kivita (mauaji, ubakaji na uporaji)  unaodaiwa kufanywa mwaka 2002-2003, katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR). 

Mawakili wake wa utetezi wanadai kwamba majeshi ya   mteja wao yalikuwa chini ya CAR wakati uhalifu huo ulipokuwa unatendeka. 

Seara aliiambia mahakama kuwa hajawahi kamwe kufika Afrika ya Kati lakini aliweza kukutana na maafisa wa jeshi wa DRC na CAR kutoa utaalamu wake katika muundo wa utoaji amri wakati wa mapambano. 

‘’Kamandi ya Operesheni ilikuwa chini ya CAR wakati wa mapambano,’’ alisema. 

Kwa mujibu wa Jenerali huyo, ilikuwa haiwezekani kwa majeshi mbalimbali yaliyopo kwenye mgogoro huo, kuwa na kamandi tofauti ya utoaji amri wakati kama huo,hali ambayo ingeleta vurugu na hata kufikia hatua ya kushambuliana, wenyewe kwa wenyewe. 

‘’ Sioni ni namna gani kungekuwepo na utoaji amri tofauti wakati lengo lilikuwa moja, kuikomboa, Bangui, na kuyarejesha nyuma majeshi ya waasi hadi mpakani mwa Chadi,’’ alifafanua Seara. 

‘’Huwezi kuamini kwamba katika mgogoro kama huo, kundi kama la MLC lilikuwa linafanyakazi peke yake. ‘’Walikuwa hawapigani vita ya wao wenyewe bali vita ambayo CAR ilikuwa inataka kurejesha upya utawala wa sheria,’’ aliongeza. 

Kesi ya Bemba ilianza kusikilizwa Novemba 2012. Ushahidi huo unaendelea kusikilizwa Jumatano. 

SM/ER/GF/NI 

© Hirondelle News Agency