04.05.12 - MAJUMUISHO YA WIKI - MWENDESHA MASHITAKA ATAKA TAYLOR AFUNGWE MIAKA 80

Arusha, Mei 04, 2012 (FH) – Mwendesha Mashitaka wa Mahakama Maalum ya Sierra Leone (SCSL) wiki hii amewasilisha maombi katika mahakama hiyo akipendekeza adhabu ya kifungo cha miaka 80 jela, dhdii ya Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor huku serikali ya Libya inapinga uhalali wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kutaka kuwashitaki, mtoto wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Saif al-Islam na aliyekuwa Mkuu wa Idara wa Usalama, Abdullah al-Senuss, kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

 

SCSL

Ataka Taylor afungwe miaka 80 jela: Mwendesha Mashitaka wa Mahakama Maalum ya Sierra Leone (SCSL) wiki hii ameiomba mahakama hiyo kumpatia adhabu ya kifungo cha miaka 80 jela, Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor ili kwendana na uzito wa mashitaka aliyotiwa nayo hatiani. Aprili 26, mwaka huu, Taylor (64) alitiwa hatiani kwa mashitaka yote 11 yaliyomkabili ikiwa ni pamoja na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu,hususan  ni kwa kuwasaidia na kuwaunga mkono waaasi wa Sierra Leone katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kati 1991 na 2002. Katika taarifa fupi ya mapendekezo ya adhabu, mwendesha mashitaka aliieleza mahakama kwamba ‘’mashitaka mazito’’ aliyotendaTayloryanastahili adhabu ya muda mrefu. Hoja hizo zitajadiliwa hadharani mahakamani Mei 16, 2012 na adhabu kutangazwa Mei 30.   

ICC

Libya yapinga ICC kuwashitaki watu wake: Serikali ya Libya inapinga uhalali wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kutaka kuwashitaki raia wake ambao ni , mtoto wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Saif al-Islam na aliyekuwa Mkuu wa Idara wa Usalama, Abdullah al-Senuss, kwa mashitaki ya uhalifu wa kivita.Katika taarifa yake, serikali hiyo imedai kwamba kuwanyima watu wa Libya nafasi hiyo ya kihistoria ya kufuta kabisa utamaduni wa watu kutoadhibiwa kwa makosa wanayofanya, itakuwa ni kinyume cha mkataba wa Roma ambayo unatambua mamlaka ya mahakama za kitaifa.Mfumo wa Mahakama za Libya, kwa mujibu wa maombi hayo, ulikuwa unawachunguza watuhumiwa hao wawili kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu, wanayotuhumiwa na ICC.

Kesi ya Bemba yaendelea kuunguruma:Mei mosi wiki hii kesi ya mshitakiwa  Jean Pierre Bemba ilingia katika awamu muhimu ambapo mmoja kati ya waathiriwa na vitendo vya uhalifu anavyokabiliwa navyo mshitakiwa huyo, alitoa ushahidi wake.Mwathiriwa huyo katika ushahidi wake aliieleza mahakama jinsi alivyobakwa na kundi la waasi la MLC.Pia alisimulia jinsi uporaji na mauaji yaliyokuwa yanafanywa na kundi hilo la waasi katika eneo alilokuwa anaishi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Senata huyo wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kiongozi wa MLC, anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita aliodaiwa kutenda katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kati ya mwaka 2002 na 2003.

NI/FK

© Hirondelle News Agency