Kajelijeli
10.12.03 - ICTR/KAJELIJELI - MEYA KAJELJELI AHUKUMIWA KIFUNGO CHA MAISHA JELA
Arusha, Desemba 01, 2003 (FH) Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR) Jumatatu imemhukimu kifungo cha maisha jela kwa muda wote uliosalia wa maisha yake, Meya wa zamani wa wilaya ya Mukingo, mkoa wa Ruhengeri nchini Rwanda Juvenal Kajelijeli baada kupatikana na hatia ya makosa matatu ya mauaji ya halaiki. Akisoma adhabu hiyo, Jaji Mtanzania William Sekule alitamka kwamba Kajelijeli ametiwa hatiani kwa makosa ya mauaji ya halaiki na ukatili dhidi ya binadamu ambapo adhabu yake kila moja ni kifungo cha maisha jela kwa muda wote uliosalia wa maisha yake.
21.11.03 - ICTR/KAJELIJELI - KESI YA MEYA WA MUKINGO KUTOLEWA HUKUMU DESEMBA
Arusha, Novemba 20, 2003 (FH) Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR) inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya mauaji ya halaiki inayomkabili Meya wa zamani wa Mukingo mkoani Ruhengeri, Juvenal Kajelijeli tarehe Mosi mwezi ujao. Msemaji wa Mahakama hiyo Roland Amoussouga alithibitisha tarehe ya kutolewa hukumu hiyo mjini hapa Jumatano.
17.07.03 - ICTR/KAJELIJELI - WAKILI WA KAJELIJELI ATAKA MTEJA WAKE AACHIWE HURU
Arusha, Julai 16, 2003 (FH) Wakati mwendesha mashtaka katika kesi ya mauaji ya halaiki dhidi ya Meya wa zamani wa wilaya Mukingo nchini Rwanda, Juvenal Kajelijeli aliiomba mahakama kumtia hatiani na kumhukumu kifungo cha maisha jela mtuhumiwa huyo, Jumatano wakili wa utetezi alitoa ombi tofauti la kutaka mteja wake achiwe huru. Wakili huyo, Profesa Lennox Hinds kutoka Marekani alitoa ombi hilo mbele ya Mahakama namba Mbili ya Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR) wakati wa kutoa hoja za mwisho za utetezi wa mteja wake.
16.07.03 - ICTR/KAJELIJELI - ATAKA KAJELJELI AFUNGWE MAISHA
Arusha, Julai 15, 2003 (FH) Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR) Jumanne ameiomba mahakama hiyo kumtia hatiani na kumpa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa muda wote uliosalia wa maisha, mtuhumiwa mmoja wa mauaji hayo, Juvenal Kajelijeli, Meya wa zamani wa wilaya ya Mukingo mkoani Ruhengeri Kaskazini Magharibi ya Rwanda. Mwendesha mashtaka huyo Ifeoma Ojemini kutoka Nigeria aliiambia mahakama hiyo katika majumuisho ya mwisho ya kesi dhidi ya mtuhumiwa huyo kwamba tuhuma zinazomkabili Kajelijeli ni nzito na adhabu anayostahili kupewa ni kifungo cha maisha kwa muda wote uliosalia wa maisha yake.
14.07.03 - ICTR/KAJELIJELI - ZIPO HOJA NYINGI ZA KUMTIA HATIANI KAJELIJELI-MWENDESHA MASHTAKA
Arusha, Julai 14, 2003 (FH) – Mwendesha mashtaka katika kesi ya mauaji ya halaiki dhidi ya Meya wa zamani wa wilaya ya Mukingo mkoani Ruhengeri (Kaskazini Magharibi ya Rwanda) ameiambia Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR) Jumatatu kwamba anazo hoja nzito zitakazothibisha pasipo wasiwasi wowote kwamba mtuhumiwa huyo alihusika na mauaji hayo ya halaiki. Mwendesha mashtaka huyo Ifeona Ojemini kutoka Nigeria alikuwa anatoa majumuisho ya mwisho katika kesi dhidi ya Meya huyo wa zamani mbele ya Mahakama namba Mbili ya mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa.
