21.04.04 - ICTR/MAJAJI - MRITHI WA JAJI WILLIAMS APATIKANA

Arusha, Aprili 20, 2004 (FH)-Jaji Charles Michael Dennis Byron kutoka visiwa vya St. Kitts na Nevis ameteuliwa kuchukua nafasi ya Jaji George Llyod Williams pia wa visiwa hivyo, aliyejiuzulu mwezi uliopita kufanyakazi katika Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR).

Msemaji wa mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa, Roland Amoussouga, Jumanne alithibitisha uteuzi wa jaji huyo.

Amoussouga aliongeza kuwa Jaji Byron aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan baada ya kushauriana na Marais wa Baraza la Usalama na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Uteuzi wake ulianza Aprili 8 mwaka huu na atafanyakazi hadi Mei 27, 2007.Kabla ya kuteuliwa kwake alikuwa ni Jaji Mkuu wa Mahakama Kuu ya Mashariki ya visiwa vya Caribian .

Jaji Byron alizaliwa mwaka wa 1943 na alianza kufanya kazi mwaka wa 1965 kama mwanasheria katika mahakama kuu ya Uingeraza na Wales.Aliwahi kushika pia nyadhifa mbalimbali katika kada za mahakama hadi alipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama kuu ya Mashariki ya Visiwa vya Caribian kati ya 1982 hadi 1990.Mnamo mwaka 1999 alipandishwa cheo na kuwa Jaji Mkuu katika visiwa hivyo.

Naye Jaji Williams (77) katika kujiuzulu kwake alidai kunatokana na sababu binafsi. Jaji huyo toka visiwa hivyo vilivyopo katika bahari ya Caribian, alichaguliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Novemba 1998 kushika wadhifa huo na alichaguliwa kwa awamu ya pili Januari 2003 kuendelea kuitumikia mahakama hiyo.

PJ/NI/FH/(ICTR''0420s)