17.09.04 - ICTR/MAJAJI - MAJAJI WAPYA WATANO WAAPISHWA ICTR
Arusha, Septemba 17, 2004 (FH)- Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) Ijumaa imewaapisha majaji watano wapya katika sherehe iliyoongozwa na Rais wa Mahakama hiyo Jaji Erik Mose.
Kuapishwa kwa majaji hao kumefikisha idadi wa majaji wote wa mahakama hii kuwa 18 ambapo wanane kati yao ni majaji wanawake.
Majaji tisa ni majaji wa kudumu na wengine tisa ni majaji wa kufanyakazi kwa muda maalum.
Majaji waliopishwa ni pamoja na Jaji wa kudumu Joseph Asoka Nihal de Silva kutoka Sri Lanka anayechukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Asoka de Zoysa Gunawardana pia kutoka nchi hiyo baada ya kujiuzulu kutokana na sababu za kiafya.
Majaji wengine wanne waliapishwa kama majaji wa muda maalum. Nao ni pamoja na Taghreed Hikmat kutoka Jordan, Karin Hokborg wa Sweden, Gberdao Gustave Kam wa Burkina Faso na Seon Ki Park kutoka Jamhuri ya Watu wa Korea.
Akiwakaribisha majaji wapya baada ya kuhitimisha kula kiapo mmoja baada ya mwingine, Rais wa mahakama hiyo Jaji Mose alisema kuwasili kwa majaji hao kutawezesha mahakama yake kusikiliza kesi nyingine mbili kuanzia Jumatatu ijayo. Kesi hizo ni pamoja na ile dhidi ya maafisa waandamizi wanne wa zamani wa jeshi la Rwanda na nyingine dhidi ya Padre wa zamani wa parokia ya kanisa katoliki ya Nyange mkoani Kibuye, Magharibi ya Rwanda, Athanas Seromba.
‘’ Hayo yote ni kwa ajili kuhakikisha kwamba uendeshaji wa kesi hizo unakuwa bora na kwa kasi inayotakikana,’’ Jaji Mose alisema na kuongeza kuwa ‘’Jumatatu ijayo kutakuwepo mahakamani jumla ya watuhumiwa 25 ambao kesi zao zitakuwa zinasikilizwa.’’
NI/FH/(JG’’0917s)


