30.11.04 - ICTR/MAJAJI - GUNAWARDANA ALIYEKUWA JAJI WA ICTR AFARIKI DUNIA
Arusha, Novemba 30, 2004 (FH)- Jaji wa zamani wa Mahakama ya Kimataifa ya Watuhumiwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) na mjumbe katika Mahakama ya Rufaa ya Mahakama hiyo, Jaji Asoka de Zoysa Gunawardana wa Sri lanka amefariki dunia Ijumaa iliyopita na mwili wake kuchomwa moto Jumatatu(jana) kwa mujibu wa mila na desturi ya mazishi ya dini ya Kibudha.
Ripoti kutoka mji mkuu wa Sri lanka, Colombo zimeeleza kuwa Jaji Gunawardana (62) aliaga dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Marehemu Jaji Gunawardana aliteuliwa kujiunga na ICTR, mwaka 1999 na alijiuzulu nafasi yake Aprili mwaka huu kutokana na matatizo ya kiafya.
Rais wa mahakama hiyo Jaji Erik Mose ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu Jaji Gunawardana akimwelezea kwamba ‘’ katika uhai wake amechangia kwa kiasi kikubwa maendelea ya sheria ya haki za kimataifa juu ya makosa ya jinai.
Katika kipindi cha miaka minne aliyofanyakazi katika ICTR alishiriki kuendesha kesi tatu kubwa za watuhumiwa wa mauaji ya halaiki ambapo moja kati yake mtuhumiwa alichiwa huru.
Mtuhumiwa aliyeachiwa huru katika kesi ambayo Jaji Gunawardana alikuwa ni miongoni mwa jopo la majaji watatu waliyosikiliza na kutoa hukumu ni ile iliyomhusu Meya wa zamani wa wilaya Mabanza mkoani Kibuye Mashaki ya Rwanda, Ignace Bagilishema.
Desemba mwaka jana Marehemu Jaji Gunawardana alishiriki katika jopo lingine la majaji watatu katika kutoa hukumu ya kihistoria dhidi ya wakuu watatu wa zamani wa vyombo vya habari nchini Rwanda akiwemo Profesa Ferdinand Nahimana aliyekuwa mwanzilishi wa Radio binafsi ya RTLM na Mkurugenzi wa zamani wa radio hiyo Jean Bosco Barayagwiza pamoja na aliyekuwa Mhariri na Mmiliki wa gazeti lenye msimamo mkali wa Kihutu la Kangura, Hassan Ngeze.
Profesa Nahimana na Ngeze walihukumiwa vifungo vya maisha jela ambapo Barayagwiza alihukumiwa kifungo cha miaka 35, jela.
Wakati anajiuzulu Marehemu alikuwa ni Jaji kiongozi katika kesi nyingine inayowahusisha mawaziri wanne wa serikali ya mpito nchini Rwanda. Kabla ya kujiunga na ICTR alikuwa Jaji katika Mahakama Kuu ya Sri lanka.
NI/KN/FH/(JD’’1130) ______


