02.06.10 - RWANDA/USA - ATAKA MMAREKANI ANAYESHIKILIWA RWANDA AACHIWE HURU MARA MOJA
Arusha Juni 02, 2010 (FH) - Wakili wa utetezi katika Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Vincent Courcelle-Labrousse Jumatatu wiki hii alitamka Mahakamani kuunga mkono juhudi zinazofanywa na mawakili wengine kumtoa nje mwanasheria wa Marekani aliyewekwa ndani nchini Rwanda kwa madai ya kukana kuwepo kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Mwanasheria huyo wa Marekani aliyekamatwa Ijumaa iliyopita alikuwa nchini Rwanda kama sehemu ya timu ya utetezi wa kiongozi wa chama cha upinzani nchini Rwanda Victoire Ingabire.
Kiongoizi huyo ambaye ni mpinzani wa utawala wa Rais Paul Kagame anatuhumiwa kwa makosa ya kukana kuwepo kwa mauaji ya kimbari, kushirikiana na makundi ya kigaidi na kuchochea mfarakano kati ya makabila.
‘'Tunaunga mkono mshikamano wa mawakili wanaojitahidi kumtoa gerezani Peter Erlinder,'' alisema wakili Courcelle-Labrousse kutoka Ufaransa.
Mwanasheria huyo ni wakili wa utetezi katika kesi ya mauaji ya kimbari inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Vijana nchini Rwanda, Callixte Nzabonimana.
Katika hoja zake anadai kwamba Profesa Erlinder amekamatwa kutokana na mhadhara alioutoa Brussels nchini Ubelgji hivi karibuni na machapisho yake juu ya mauaji ya kimbari na siyo kwa madai ya matamshi yaliyotolewa na mwanasheria huyo nchini Rwanda.
‘'Hakutoa matamshi yoyote nchini Rwanda ambayo yanaendana na tuhuma anazokabiliana nazo,'' alilieleza jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Solomy Balungi Bossa wa Uganda.
Wakili huyo pia alichukua nafasi hiyo kuieleza mahakama jinsi yeye na mpelelezi katika kesi yake walivyotiwa mbaroni na maafisa wa Rwanda kwa saa 12 walipoingia nchini humo mwaka 2008 kufuatilia kesi ya mteja wao Nzabonimana.
‘'Mpelelezi wetu alilazimika kuikimbia Rwanda kabla hata kesi ya mteja wetu haijakamilika,'' alilalamika Wakili huyo.
Akijibu hoja hizo, Mwendesha Mshtaka Mwandamizi wa ICTR, Paul Ng'arua kutoka Kenya alimshutumu wakili huyo kutumia tukio hilo la kukamatwa kwa wakili Erlinder kuelezea kisa chake.
‘'Wakili wa Nzabonimana hajawahi kuwasilisha mahakamani hoja yoyote kwamba alinyayaswa na serikali ya Rwanda,'' alisema.
Muda mfupi kabla mahakama haijaendelea na kusikiliza shahidi wa utetezi, Jaji Bossa alisema mahakama yake imepokea hoja zilizotolewa na pande zote mbili na pia kumtaka wakili wa utetezi kuijulisha mahakama iwapo utakabiliwa na tatizo lolote katika uendeshaji wa kesi yake.
Profesa Erlinder ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Utetezi ICTR na Wakili wa utetezi wa Meja Aloys Ntabakuze ambaye anasubiri kusikilizwa kwa rufaa yake baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa.
NI
© Hirondelle News Agency


